KESHA LA ASUBUHI
ALHAMISI, NOVEMBA 24 2022
ILI KUILISHA ROHO, ZUNGUMZA NA YESU KILA SIKU
Hakuna wakala wa kibinadamu anayeweza kutoa kile ambacho kitatosheleza njaa na kiu ya nafsi. Lakini Yesu asema, "Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami." (Ufunuo 3:20). "Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe" (Yohana 6:35).
Kama vile tunavyohitaji chakula ili kudumisha nguvu zetu za kimwili, ndivyo tunavyomhitaji Kristo, Mkate utokao mbinguni, kudumisha maisha ya kiroho na kutoa nguvu za kufanya kazi za Mungu. Kama vile mwili unavyodumu kupokea lishe ambayo inahimili uhai na nguvu, ndivyo ambavyo ni lazima roho iwe inawasiliana na Kristo kila wakati, ikijinyenyekesha kwake na kumtegemea kabisa.
Kama vile msafiri aliyechoka anavyotafuta chemchemi jangwani na, anapoipata, anazima kiu yake kali, ndivyo ambavyo Mkristo ataona kiu na kupata maji safi ya uzima, ambayo kwayo Kristo ndiye chemchemi.
Pale tunapotambua ukamilifu wa tabia ya Mwokozi wetu tutatamani kubadilishwa kikamilifu na kufanywa upya katika sura ya usafi Wake. Kadiri tunavyomjua Mungu zaidi, ndivyo ambavyo mfano wetu wa tabia bora utakavyokuwa wa juu na ndivyo shauku yetu ya kuakisi sura yake itakavyokuwa yenye bidii zaidi. Asili ya kiungu inaungana na mwanadamu wakati roho inapomtafuta Mungu na moyo wenye shauku unaweza kusema, "Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake." (Zaburi 62:5).
Ikiwa una hisi ya uhitaji ndani ya roho yako, ikiwa unaona njaa na kiu ya haki, huu ni ushahidi kwamba Kristo ametenda kazi moyoni mwako, ili apate kutafutwa kwa ajili ya kukutendea, kwa majaliwa ya Roho Mtakatifu, mambo yale ambayo haiwezekani kwako wewe mwenyewe kujitendea....
Maneno ya Mungu ndiyo chemchemi za maisha. Kadiri unavyotafuta chemchemi hizo zilizo hai, kwa njia ya Roho Mtakatifu, utaletwa katika ushirika na Kristo. Kweli zilizozoeleka zitajidhihirisha akilini mwako katika sura mpya, aya za Maandiko zitafunguka ghafla kwako kama mwako wa nuru zikiwa na maana mpya, utaona uhusiano wa kweli nyingine katika kazi ya ukombozi, na utajua kwamba Kristo anakuongoza, Mwalimu wa kiungu yuko kando yako. -Thoughts from the Mount of Blessing, 18-20.
ILI KUILISHA ROHO, ZUNGUMZA NA YESU KILA SIKU
Reviewed by Inspirit Academy
on
noviembre 23, 2022
Rating:
No hay comentarios: